Mkutano wa Mashirikiano ya Pamoja baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Oman

Lengo : Kuondosha changamoto ya upatikanaji wa maji na umeme katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar e-Government Said Seif Said aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa pamoja baina ya serikali na Wataalamu kutoka Oman katika masuala ya maji na umeme katika ukumbi wa Verde Mtoni. Aidha alisema mkutano huo una manufaa makubwa katika kutafuta njia bora za kuwezesha Zanzibar katika uendelevu wa masuala ya kidigitali hasa maji na umeme. Mkurugenzi Said alibainisha kuwa pia mkutano huo utatoa fursa kwa ZAWA kueleza changamoto zilizokuwepo ili wadau kutoka Oman na Afrika Kusini waliobobea katika masuala hayo kuwapa njia ambazo zitasaidia kuondosha changamoto hizo na kuingia katika utaratibu mzuri za kuhudumia masuala ya umeme na maji. “Naamini baada ya mkutano huu nasi Zanzibar tutaondokana na kutumia njia za kawaida na badala yake kutumia teknolojia katika kutoa huduma bora, ikiwemo Mfumo kuweza kuona bomba la maji likiharibika popote bila ya mwananchi kuripoti kama ilivyo sasa, na hii itarahisisha usimamizi katika kutoa huduma za maji na umeme kwa umma,” alibainisha. Naye Ali Abdullah Al Maskery kutoka National Energy Center ya nchini Oman, alisema wameamua kubadilishana uzowefu walionao na serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) katika masuala ya maji ili kuona Zanzibar inaondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali. Hivyo waliahidi kushirikiana pamoja katika kuona mradi huo unaanza mara moja ili kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi. Mapema Mahomoud Omar Makame kutoka Mamlaka ya Maji ZAWA alisema hivi sasa mamlaka hiyo inatarajia kubadilisha mfumo wa zamani na kuingia mfumo mpya wa kidigital hivyo wapo katika kubadilishana uzoefu ili kuona wanapata uzoefu katika masuala hayo. Alisema ikiwa watatoka katika mfumo wa zamani na kuingia katika mfumo mpya basi asilimia kubwa ya changamoto ya maji itaondoka na kumalizika kabisa. Hivyo aliwaomba wananchi wa Zanzibar kuwa tayari na kutarajia mambo mazuri ambayo yataiwezesha ZAWA kufanya mabadiliko makubwa katika sekta hiyo ya maji nchini.   Mkutano huo wa siku moja pia ulishirikisha kampuni nyengine zilizobobea katika masuala ya maji na umeme kutoka Afrika Kusini.