Wakala wa Serikali Mtandao ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sheria nambari 12 ya mwaka 2019 yenye jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma
Wakala wa Serikali Mtandao una muundo ufuatao,
- Bodi ya ushauri ya Wakala wa Serikali Mtandao
- Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
- Idara, Divisheni na Vitengo
Bodi ya ushauri wa Wakala wa Serikali Mtandao
Bodi inaongozwa na mwenyekiti aliyeteuliwa na Rais na wajumbe ambao wameteuliwa na waziri kulingana na sifa zilizoainishwa katika sheria ya Wakala wa Serikali Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
Mkurugenzi Mtendaji ambae ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala na ana wajibu wa kusimamia utendaji wa kazi za kila siku na uongozi wa Wakala.
Idara, Divisheni na Vitengo
Wakala wa Serikali Mtandao ina Idara tano (5) ambazo zinaongozwa na Wakurugenzi ambao wanaripoti moja kwa moja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala. Idara hizo ni kama zifuatazo:
Idara ya Rasilimali Watu, Utawala na Mipango
Lengo la Idara hii ni kutoa huduma za Uendeshaji, Utawala, Rasilimali watu na Mipango ya Wakala ya kila siku, pamoja na kutunza, kuhuisha na kuhifadhi kumbukumbu.
Idara ya Usimamizi wa Huduma za TEHAMA
Idara ina majukumu ya kutoa utaalamu na ushauri katika utoaji wa huduma za serikali mtandao, kufanya utafiti, kujenga uwezo na kukuza ubunifu juu ya mipango ya Serikali Mtandao. Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, viwango, miongozo na miradi ya TEHAMA kwenye taasisi za Umma.
Idara ya Uchambuzi na Usanifu wa Mifumo
Idara ina jukumu la uchambuzi, utengenezaji pamoja na uunganishwaji wa mifumo ya kielektroni yenye gharama nafuu na salama kwa maslahi ya umma.
Idara ya Usimamizi wa Miundombinu ya TEHAMA
Idara ina jukumu la kusimamia miundombinu ya TEHAMA, usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya Wakala na mifumo jumuishi ya utoaji wa huduma za Serikali kielektroniki, kuhakikisha usalama wa mifumo na vifaa vya TEHAMA katika Taasisi za Umma.
Ofisi ya Uratibu Pemba
Idara ina na jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli zote za Wakala wa Serikali Mtandao kwa Pemba pamoja na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya Uendeshaji wa Wakala. Katika kutekeleza majukumu yake Wakala wa Serikali Mtandao Pemba inaongozwa na Afisa Mratibu wa Wakala ambae ameteuliwa na Mkurugenzi Mtendaji.