Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kusimamia na kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za umma kwa njia ya mtandao, ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mamlaka hii ilianza kama Idara ya Habari na Mawasiliano, ikiwa chini ya Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar. Baadae, Serikali ilichukua hatua ya kuibadilisha Idara hiyo kuwa Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar, kupitia Sheria Namba 12 ya Mwaka 2019, ili kuimarisha usimamizi wa TEHAMA katika utumishi wa umma.
Kutokana na mafanikio na ufanisi mkubwa wa Wakala wa Serikali Mtandao katika kuratibu na kusimamia matumizi ya TEHAMA serikalini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliona haja ya kuipa taasisi hiyo mamlaka kamili na nguvu zaidi kisheria. Hivyo, mnamo mwaka 2024, Serikali ilifuta Sheria ya Wakala wa Serikali Mtandao (Na. 12 ya 2019) na kutunga Sheria Mpya Namba 1 ya Mwaka 2024, ambayo ilianzisha rasmi Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ).
Sheria hii mpya imeipa eGAZ jukumu la kusimamia huduma za Serikali Mtandao Zanzibar na masuala yote yanayohusiana na TEHAMA katika sekta ya umma. Madhumuni ya kuanzishwa kwa Mamlaka hii ni:
- Kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kupitia TEHAMA;
- Kuweka mfumo madhubuti wa uratibu, usimamizi na utekelezaji wa sera, miongozo na viwango vya TEHAMA serikalini;
- Kuendeleza dhamira ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kuifanya Zanzibar kuwa jamii ya kidijitali (“Zanzibar ya Kidijitali”).
Kwa msingi huo, eGAZ inafanya kazi kama chombo kikuu cha kitaifa kinachotoa muongozo, ushauri na uratibu wa matumizi ya TEHAMA katika taasisi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa mabadiliko ya kidijitali unaolenga kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia teknolojia.
Dira
Kuwa kitovu cha utaalamu na ubunifu chenye kurahisisha upatikanaji wa huduma za TEHAMA serikalini
Dhamira
- Kutumia teknolojia kwa ubunifu ili kuwezesha maendeleo ya huduma zinazomjali mwananchi, kuendeleza usawa kwa wote, na kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora bila vikwazo.